HISTORIA: Wabulushi na Ngome ya Fort Jesus Mombasa

0

Kitabu hiki cha Historia kimeandikwa na

Ali Jumadar Amir

MOMBASA

UTANGULIZI

Mimi mwandishi wa Historia hii ya Wabulushi na Ngome ya Fort Jesus Mombasa, nimepata kusoma vitabu ambavyo vimehusika na Historia ya Pwani ya Afrika Mashariki kabla ya kufika kwa Wareno na baada ya kufika kwa Wareno.  Nikiwa malimu wa shule, nimepata kuifunza Historia ya Pwani ya Afrika Mashariki shuleni.  Habari nilizopata vitabuni zimenisaidia katika uwandishi huu.

Vile vile nimepata kusikia na kupokea habari nyingi kuhusu Historia ya Mombasa na mambo yaliyotokea hapo kale.  Miongoni mwa watu walionisaidia kunipa habari hizi za Wabulushi, walikuwa hawa wafuatao:-

Shukrani zangu ziwafikie.

1.               Sheikh Ali Mohamad bin Yunus

                  Tamimu Thalatha Twaifa MOMBASA

2.              Sheikh Hussein Ahmed Baluchi

3.              Sheikh Mohamad Kamal Khan Baluchi

4.              Sheikh Kher Mohamad Ali Baluchi

5.              Sheikh Sudi Suleiman Mirza Baluchi

6.              Sheikh Ahmad Mohamad Khamis Shapiy Baluchi

WABULUSHI NA NGOME YA FORT JESUS MOMBASA

Katika mwaka 1590 A.D.  Wareno waliwashinda Waswahili wa Mombasa vitani na wakaukamata mji wa Mvita.  Vita vyao vilikuwa vya siku nyingi.  Katika kuendesha utawala wao hapo Kisiwani, mambo hayakuwa mazuri.  Palitokea vita vya kuviziana baina ya Wareno na Waswahili wa Mombasa.  Vita hivyo viliendelea usiku na mchana.  Wareno hawakuweza kutawala vizuri hapo kisiwani, Mombasa.

Kwa sababu ya vifo vingi na amani kukosekana, mnamo mwaka 1592 A.D. Wareno waliijenga ngome hii na wakaita Fort Jesus.  Ngome hii ilijengwa kivita.  Waliitumia ngome hii kwa kujihami nafsi za vitani.   Baada ya kuijenga ngome hii ya vita, Wareno walipata nafasi ya kuuendesha utawala wao hapo kisiwani, Mombasa, palipotokea vita walikimbilia humo kujificha.

Baada ya kuijenga ngome hii, Wareno waliwatesa na kuwaadhibu Waswahili wa mji wa Mombasa.  Katika kuuendesha utawala wao, Wareno waliwatilia Waswahili wa Mvita vikazo vingi na masharti mengi katika kuuendesha utawala wao hapo kisiwani.  Utawala wao haukuwa na busara zaidi walitumia taadi, nguvu na ubora. Mtu akiwa ajipenda na kujivuna sana,  Waswahili husema.  “Mtu Fulani ajipenda kama Mreno”.

Watu huru siku zote huwa hawapendi kutawaliwa vibaya.  Waswahili katika miji ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki walipata habari ya kushambuliwa kwa Wareno na kutolewa katika nchi ya Maskat Omani.  Kwa kuwa wao walikuwa waislamu na walichokana na utawala wa Kireno, waliazimu kwenda kuomba msaada kwa Waislamu ndugu zao huko Maskat Omani.  Waliwataka Waarabu wa Maskat Omani wawasaidie katika kuwaondowa Wareno mijini mwao katika Pwani ya Afrika Mashariki.  Siku hizo mtawala wa nchi ya Maskat Omani alikuwa Imam Sultan Bin Seif Bin Malik Yurbi, maarufu alijulikana kwa jina la Keidil Ardhi.  Yeye na majeshi yake ya Waarabu na Wabulushi waliwaondoa Wareno nchini mwao, mnamo mwaka 1650 A.D.

Mnamo mwaka 1661, Waswahili wa Mombasa waliwapeleka wajumbe wao Maskat Omani kuomba msaada kwa Imam Sultan Bin Seif Bin Malik Yurbi, walimtaka yeye awasaidie kuwaondoa Wareno mjini mwao.  Mtawala huyo aliwafahamu sana watu wa Mombasa kwa sababu ya biashara iliyokuwapo baina ya nchi ya Maskat Omani na Waswahili wa Mombasa.  Keidil Ardhi alijua kwamba hapo mbeleni wote walikuwa wametawaliwa na Wareno.  Keidil Ardhi alizifahamu vizuri taadi na jeuri za Wareno.  Baada ya mazungumzo yao marefu, Imam  Sultan Bin Seif Yurbi alikubali kuwasaidia Waswahili wa Mombasa, katika  kuwaondoa Wareno mjini mwao.

Habari za ushindi wa Keidil Ardhi katika kuwatoa Wareno nchini mwao zilienea katika miji ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki.  Waswahili kutoka miji ya kale ya hapo, waliwapeleka wajumbe wao kuomba msaada wa kuwaondoa Wareno katika miji yao huko Maskat Omani.  Kwa kuwa wao walikuwa Waislamu, Sultan Bin Seif Bin Malik Yurbi alikubali kuwasaidia.

Baada ya kuongea na watu wake na wakuu wa majeshi yake, Keidil Ardhi alimchagua Amir Jumadar Shahdad Chotah kuitayarisha na kuendesha kazi hiyo.   Alimuamini sana Amirjeshi huyu wa Kibulushi kwa ushujaa wake.  ALiziona harakati zake katika vita hapo nchini pake, Maskat Omani.  Imam Sultan Bin Seif Yurbi aliwaarifu Waswahili katika miji ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki habari ya shujaa huyo.  Vile vile aliwataka wamsaidie Amirjeshi huyo katika kuiendesha kazi yake afikapo mijini mwao.

Kabla ya kuzijua nguvu za Wareno, Amir Jumadar Shahdad Chotah hakuamini kuyapeleka majeshi yao bila ya kuzijua nguvu za Wareno katika Pwani ya Afrika Mashariki.  Alijitolea mwenyewe kufika Pwani ya Afrika Mashariki akiwa jasusi.  Alifika katika Swahilini ya Afrika Mashariki na akafanya ujasusi katika miji ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki akisaidiwa na wenyeji wa miji hiyo.  Katika ujasusi wake, Amir Shahdad Chotah alijifanya mfanyi biashara ili Wareno wasimjue.

Amir Jumadar Shahdad Chotah alifika Mombasa.  Alifanya kazi yake ya ujasusi hapo kisiwani akisaidiwa na Waswahili wa mji wa Mombasa.  Wareno walimuona na wakamfanyia shaka, walimkamata wakamfunga humo ngomeni.  Katika kujitetea alidai kwamba yeye alifika hapo akiwa mfanyi biashara.  Wareno hawakuwa wakimjua.  Humo kifungoni ngomeni, Amir Shahdad Chotah alifanya ujasusi vile vile.  Alifungwa humo kwa muda halafu akaachiliwa.  Huyo alikuwa Bulushi wa kwanza kufungwa katika ngome hii.  Amir Jumadar shahdad Chotah aliondoka Mombasa akarudi Maskat Omani akiwa ana ujuzi wa nguvu  za Wareno katika Pwani ya Afrika Mashariki.

Hapo Maskat Omani baada ya kufika huko salama, Amir Jumadar Shahdad Chotah aliyatoa maonyi yake kuhusu nguvu za Wareno katika Pwani ya Afrika Mashariki.   Imam Sultan Bin Seif Bin Malik Yurbi aliyasikiliza vizuri maonyi ya Amirjeshi huyo na akakubali kumpatia majeshi, silaha, chakula na vyombo vya kubeba askari na silaha zao.   Alimuamuru Shahdad Chotah kuwashambulia Wareno katika miji ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki na kuwaondoa Wareno katika miji hiyo.  Amir Jumadar Shahdad Chotah alikubali kuyachukuwa madaraka hayo.

Mnamo mwaka 1664 A.D.  chini ya uwamiri wa Jumadar Shahdad Chotah majeshi ya Imam Sultan Bin Seif Yurbi yaliondoka Maskat Omani yakaelekea Pwani ya Afrika Mashariki.

Miongoni mwa majeshi hayo walikuwa askari wa Kiarabu na wa kibulushi.  Majeshi hayo yalipofika hapa, askari waliyashambulia mamlaka ya Wareno katika miji ya kale ya hapo.  Waliwaondoa Wareno katika miji ya Pate, Lamu, Barawa, Moghdisho, Malindi na miji mengine midogo midogo.  Kwa kuogopa kukamatwa na kuwa mahabusu, Wareno walikimbilia kujificha kwenye ngome hii kubwa ya Fort Jesus hapa Mombasa.  Wareno wengine walienda Msumbiji kuishi na jamaa zao.  Wale waliokamatwa walifanywa mahabusu.  Amir Jumadar Shahdad Chotah aliwaeka askari wa ulinzi katika miji hiyo wakiwa wa Kiarabu na wa Kibulushi.

Katika kuwashambulia Wareno hapo mjini Mombasa, palitokea vita vikali, Wareno walipigana na majeshi kutoka Maskat Omani.   Waswahili wa mji wa Mombasa walilwasaidia Waomani vitani.   Wareno hawakuwa wakipata msaada kwa njia ya bahari.  Walipozidiwa nguvu, walijihami na wakajificha humo ngomeni.  Waswahili wa Mombasa waliwaonyesha askari kutoka Omani vipembe vyote vya Wareno vya kuweza kutorokea.  Vivukoni waliwekwa askari na ulinzi.

Wareno walizidiwa nguvu hapa Mombasa.  Walijificha humo ngomeni na lango la ngome hiyo wakalifunga, walibaki kuishi humo mpaka chakula kikawaishia.  Baadhi walikufa kwa njaa na wengine walikufa kwa maradhi.   Hali ilipozidi kuwa mbaya na hawakuwa wakipata msaada, Wareno walilifungua lango la Fort Jesus na wakajitolea.

Amir Jumadar Shahdar Chotah na majeshi yake aliwashinda Wareno vitani na akaikamata ngome hii ijulikanayo kwa jina la Fort Jesus.  Baada ya ushindi huo, Amirjeshi huyo aliwaeka askari wa ulinzi wa mji wa Mombasa humo ngomeni.  Miongoni mwa askari hao walikuwa Wabulushi na Waarabu.   Siku hizo, Waarabu hao walijulikana kwa jina la Mazurui.

Amir Jumadar Shahdad Chotah na majeshi yake, aliwashinda Wareno katika Pwani ya Afrika Mashariki.   Wareno walitolewa katika miji ya kale ya hapo wakabaki kuishi Msumbiji na Goa.  Katika miji ya kale ya Pwani  Mashariki, alieka ulinzi wa kuweza kupambana na Wareno walipojaribu kufika hapo.   Katika kila ngome ya vita aliwaeka askari wa Kiarabu na wa Kibulushi.   Amirjeshi huyu katika kuiendesha kazi yake alikuwa akiona mbali.  Hapa Pwani ya Afrika Mashariki, Amir Jumadar Shahdad Chotah aliishi katika ngome hii ya Fort Jesus hapa, Mombasa.  Alifanya ziara……………………………………………………

Kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuwaondoa Wareno ambao wakiwatesa sana watu katika miji ya kale, Jamadari mkuu huyu wa vita alipendwa sana na Waswahili wa Mijimitatu wa Mombasa ambao walipigana na Wareno kuanzia mwaka 1500 A.D. hadi mwaka 1664 A.D. walipopata msaada kutoka kwa Imam Sultan Bin Seif Bin Malik Yurbi aliyekuwa mtawala wa nchi ya Maskat Omani siku hizo.

Wakilindini walisifika kwa ushujaa hapo Mvita.  Mtawala katika Mijimitatu siku hizo alikuwa Ahmad Mwinyi Mbwana Mkilindini.  Kwa sababu ya mapenzi na furaha, Amir Jumadar Shahdad Chotah aliozwa Fatuma Binti Ahmad Mwinyi Mbwana binti ya mtawala wa Mijimitatu.  Hapo Mombasa Amir Jumadar Shahdad Chotah alizaa mtoto wa kike.  Binti huyo baadaye aliolewa na jamaa zake, Wakilindini.

Vita katika Pwani ya Afrika Mashariki viliendelea.  Wareno walipopata nguvu walirudi kuikomboa miji waliokuwa wameikamata. Waliweza kuikomboa baadhi ya miji hiyo lakini hawakuweza kukaa humo kwa muda mrefu.  Waomani wakisaidiwa na Waswahili wa miji hiyo, waliweza kuwashinda Wareno na …………………..

Mnamo mwaka 1668 A.D.  Imam Sultan Bin Seif Bin Malik Yurbi alifariki dunia.   Utawala wa Maskat Omani mara hii ulirithiwa na mtoto wake Seif Bin Sultan Bin Seif Yurbi.  Mtoto huyo hakubadili nia.  Aliendelea kupigana na Wareno mpaka wakawashinda.  Wareno walibaki kuishi Msumbiji na Goa.  Wabulushi waliendelea kuwa walinzi katika miji ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki kutoka karne ya 17.  Waliishi katika ngome zilizojengwa na kuachwa na Wareno kuanzia Pwani ya Somalia hadi Tungi katika pwani ya Tanzania.

Mnamo mwaka 1712 A.D. Imam Seif bin Sultan Yurbi alikufa hapo Maskat Omani.  Baada ya mtawala huyo kufa, palitokea vita hapo nchini Omani.  Waarabu wa nchi hiyo hawakuwa wakikubaliana kupewa Uimam mtoto wa Imam Seif bin Sultan, vita vya kikabila vilianza hapo Maskat Omani.  Waarabu walipigana wao kwa wao.  Amri kuhusu utawala wa Pwani ya Afrika Mashariki hazikuwa zikija.  Siku hizo zaidi watu wa nchi hiyo walishughulika na vita vya huko na hapakuwa na maasiliano baina ya Pwani ya Africa Mashariki na nchi ya Maskat Omani kwa muda mrefu.  Ilisadifu hapa Mvita na kisiwa cha Pemba, askari jeshi wengi walikuwa Waarabu kabila la Kimazrui na Liwali wa Mombasa, siku hizo alikuwa Nassir bin Abdalla Mazrui.   Mazrui wa Mombasa na wa Pemba walimkubali Nassir bin Abdalla kuwa Shekhe wao.  Kimnya kilipozidi na majeshi yakijiendesha yenyewe na yakisaidiwa na wenyeji wa miji ya kale ya pwani ya Afrika Mashariki.  Mazrui waliazimu kujitenga na utawala wa Maskat Omani. Hapa Mombasa Mazurui waliwashauri askari wa kibulushi na wakawataka wawaunge mkono katika mipango yao lakini Wabulushi walikataa na wakakubali kusubiri matokeo ya vita vya Maskat Omani. Mambo yalipokuwa yamefika hali hiyo na hapakuwa na masikizano baina yao, Mazrui waliwashambulia Wabulushi katika Nogme hii ya Fort Jesus na katika  kisiwa cha Pemba.  Mazrui waliwashinda Wabulushi katika vita hivyo.  Waliwatoa askari wa Kibulushi katika  Ngome hii ya Fort Jesus na Mazrui wakawa watawala wa Kisiwa cha Mombasa na kisiwa cha Pemba.   Wabulushi katika kipindi hichi waliishi hapa Mombasa na Pemba kama raia.  Hapo Mombasa Wabulushi hao waliowana na Waswahili wa Kimvita.

Katika miji mengine ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki isiyokuwa Mombasa na Pemba, Wabulushi walibaki kuishi katika ngome za miji hiyo wakiwa walinzi.  Katika kusubiri kwao, walisaidiwa na Washwahili wa miji hiyo.

Katika mwaka 1738 A.D.  vita vya kikabila vilimalizika katika nchi ya Maskat Omani hapo Arabuni.  Sultan Bin Murshid alichagulliwa kuwa Imam wa Maskat Omani.   Imam huyu alijaribu kuyarejesha mahusiano baina ya Pwani ya Afrika Mashariki na Maskat Omani.

Mnamo mwka 1741 A.D.  Imam Sultan Bin Murshid alikufa hapo Mastak Omani hapo Arabuni.  Sultan bin Murshid alichaguliwa kuwa Imam wa Maskat Omani.  Imam huyu alijaribu kuyarejesha mahusiano baina ya Pwani ya Afrika Mashariki na Maskat Omani.  

Mnamo mwaka 1741 A.D.  Imam Sultan bin Murshid alikufa hapo Maskat Omani.   Baada ya kufa mtawala huyo aliekua Ahamad Bin Said Albusaid.  Hadhi ya Imam kwa watawala hao iliondoka badili yake ikatumika ile ya Sayid.

Mnamo mwaka 1775 A.D.  Sayid Ahmed Bin Said Albusaid alifariki dunia.  Baada ya kufa mtawala huyu palitokea vita vya kikabila hapo Maskat Omani.  Waarabu walipigana wenyewe kwa wenyewe.

Baada ya vita hivyo kumalizika, mnamo mwaka 1804 A.D.  alichaguliwa Said Bin Sultan Albusaid kuwa mtawala wa nchi ya Maskat Omani.  Sayid Said Bin Sultan katika utawala wake aliazimu kuyaregesha mahusiano baina ya miji ya Pwani ya Afrika Mashariki na Maskat Omani.  Mtawala huyo alisifika kwa ushujaa na uhodari.  Alipata kukpigana vita vingi huko Maskat Omani na askari wake walikuwa Wabulushi na Waarabu.  Mmoja katika waamirijeshi wake ………….

Mashujaa hawa walikuwa wakipigana vitani bega kwa bega na wakisaidiana huko Arabuni.

Mara nyingi majeshi kutoka Maskat Omani yalishambulia mamlaka ya Mazrui hapa Mombasa na Pemba lakini hayakuwa yakifaulu.  Siku hizo za vita, Mazurui walisaidiwa sana na Waswahili wa Mijimitatu vitani.

Mnamo mwaka 1828 A.D.  Sayid Said Bin Sultan na majeshi yake kutoka Maskat Omani yalirudi kushambulia Mazrui katika mji wa Mvita.  Siku hizo Liwali wa mji huo alikuwa Salim Bin Hemed Mazurui.    Nguvu za Sayid Said Bin Sultan mara hii zilikuwa kubwa.  Baada ya vita vikali kutokea, majeshi ya Sayid Said Bin Sultan yaliweza kuwashinda Mazurui na kuukamata mji wa Mvita na Ngome ya Fort Jesus.  Waliekwa askari wa Kibulushi katika Ngome ya Fort Jesus kuulinda mji huo.  Aliekwa Amir Mohamed Shahow kuwa Jumadari mkuu wa askari hao katika Fort Jesus.

Baada ya muda kupita, Mazurui walirudi kuwashambulia askari wa ulinzi wa Sayid Said Bin Sultan katika Fort Jesus hapo Mvita.  Katika vita hivyo Mazurui walisaidiwa na Waswahili wa kisiwa hicho na Wamijikenda.  Askari wa Sayid Said Bin Sultan waliongozwa na jumadari Amir Mohamed SHahow wali……………………

Walipozidiwa nguvu walijihami katika Fort Jesus, waliendelea kupigana lakini baadaye waliishiwa na chakula humo ngomeni na hawakuweza kutoka nje.  Askari wengi katika hao walikufa kwa maradhi na njaa.  Jumadar Shahow na baadhi ya jamaa zake wa Kibulushi walipata nafasi wakatoka humo ngomeni.  Jumadar Shahow aliondoka Mvita akaenda Unguja kuipeleka habari hiyo ili imfikiye Sayid Said Bin Sultan, huko Maskat Omani.

Mazurui baada ya kushinda katika vita hivyo, walibaki watawala wa mji wa Mvita.

Mnamo mwaka 1832 A.D.  Sayid Said Bin Sultan ALbusaid alihamia Unguja yaani Zanzibar kupigana na Mazurui hapa Mombasa na Pemba.  Majeshi yake yalishinda na yaliweza kukikamata kisiwa cha Mombasa na Ngome hii ya Fort Jesus.  Majeshi hayo hayakuwa yakiweza kukaa hapo kwa muda mrefu.   Mara kwa mara walishambuliwa na Mazurui na Waswahili wa Mijimitatu na kuondolewa.

Vita hivyo viliendelea kwa siku nyingi.

Mnamo mwaka 1835 A.D.  Liwali wa Kimazrui hapa Mombasa alikuwa Khamis Bin Hemed.  Sharia zake zilikuwa ngumu hapo mjini Mombasa.  Aliyavunja masharti yaliyokuwapo baina ya Waswahili wa Mombasa na Mazurui na pakatokea hasama baina ya Mazurui na Waswahili wa Kimvita,  mara hii Waswahili walikataa kuwasaidia Mazurui vitani.  Waliwaacha pekeyao kupigana na majeshi ya Sayid Said Bin Sultan Albusaid hapa kisiwani, Mombasa.

Mnamo mwaka 1837 A.D.   Sayid Said Bin Sultan Albusaid aliwashinda Mazrui vitani.  Katika ngome hii ya Fort Jesus aliwaeka askari wa Kibulushi kwa ulinzi wa mji wa Mombasa.  Alimchagua Jumadar Tangai Bin Shambe kuwa mkuu wa askari hao na akampa madaraka kamili ya ulinzi wa mji wa Mombasa.

Mnamo mwaka 1895 A.D.  Sayid Hemed Bin Thween aliyekuwa Sultan wa Zanzibar, mamlaka yake katika Pwani ya Afrika Mashariki aliyatia katika Himaya ya Ulaya Kiingereza.  Kwa amri ya Sultan huyo wa Zanzibar iliwabidi askari wake wote kutoka kwenye ngome zilizohusika na kuwapa maafisa wa Kiingereza funguo zote za ngome hizo.  Hapa Mombasa mkuu wa ngome hii ya Fort Jesus siku hizo alikuwa Jumadar Ebrahim, kwa amri ya Sultan huyo wa Zanzibar, askari wote wa Kibulushi walitoka katika ngome hii wakabaki kuishi nje.

Jumadar Ebrahim alimpa afisa wa Kiingereza funguo zote za Ngome hii ijulikanayo kwa jina la Fort Jesus.

Hapo Mombasa Wabulushi wote baada ya kutoka katika Ngome ya Fort Jesus waliishi hapo Kibokoni karibu na Aga Khan Secondary School.   Katika kiwanja hicho kwa leo pamejengwa Central Bank of Kenya yaani Benki kuu ya Jamhuri ya Kenya.  Walikaa hapo kusubiri amri ya kurudi kwao, Maskat Omani.   Wale waliohusika kuifanya kazi hiyo hawakuwatimizia mradi wao.  Wabulushi baada ya kusubiri hapo kwa muda mrefu walimuhukumia Mungu wakasema “Alaysallah Beahkamil Hakimiin”.

Baadaye waliondoka hapo wakaenda kwenye uwanja wa Makadara.  Katika kungoja kwao hapo na walitakalo halikuwa, Wabulushi walisema “Makadara Rahman”.   Makadara Rahman maana ya kusema hivyo waliamini Mungu aliwakadiria na akawataka waishi katika mtaa wa Makadara.  Walinunua viwanja na wakajenga nyumba zao na kuishi hapo.  Baadaye walibariki kizazi wakaendelea kujenga nyumba zao katika mitaa ya Kibokoni, Miembeni na mitaa ya Pwani na kadhalika.

Siku za utawala wa Kiingereza, kwa amri ya Sultan wa Zanzibar, Wabulushi waliwasafirisha wavumbuzi wa Kizungu katika nchi za Afrika Mashariki.  Siku hizo safari zilikuwa za miguu.  Miongoni mwa wavumbuzi hao walikuwa kina Richard Button, Speka, Stanly na wengineo.  Kazi ya wavumbuzi hao wa kizungu ilikuwa kufanya uvumbuzi kwenye mito, maziwa na miteremko ya maji hapa Afrika Mashariki na kueka habari hizo katika ramani za nchi hizo.  Wabulushi waliwaongoza na kuwalinda watu hao humo safarini.

Hapa Pwani ya Afrika Mashariki, askari wa Kibulushi hawakuja na wake zao.  Waliowana na Waswahili katika miji ya kale ya Pwani ya Afrika Mashariki na wakazaana nao.  Mchanganyiko wa damu hizo ilisababisha watoto wao kuongea lugha ya Kiswahili majumbani mwao na katika arusi zao walipiga na kucheza ngoma za Kiswahili.  Utamaduni wao ni kama ule wa Kiswahili.  Hapa Mombasa Wabulushi ni miongoni mwa watu wa Kimvita.  Katika umiji wana ada na upatu wao kama wamiji wengine wanapohudhuria katika arusi za Kiswahili.

Baada ya Wabulushi kutoka katika ngome ya Fort Jesus na kuishi hapa Mombasa, walifanya kazi zao za biashara.  Siku hizo safari zilikuwa za miguu. Walisafiri na wakafika katika nchi za Uganda, Zaire, Tanzania, Kenya na Ethiopia kwa ajili ya biashara.   Waliziendesha biashara zao katika nchi hizo na baadaye walirudi katika maskani yao hapa Mombasa.

Mula Murad alikuwa mmoja katika wasafiri hao wa bara.  Yeye alikuwa mfanyi biashara  na mtangazaji wa Dini ya Kiislamu na kujenga misikiti.  Alifika Ukikuyuni, Umasaini, Ukambani na kadhalika.

Wabulushi vile vile walioa makabila ya watu wa bara kama Waganda, Wakamba, Wazire na makabila ya Kitanzania kama Wazaramu, Wanyamwezi na kadhalika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *